Wednesday, June 6, 2007

TANGA TUNAWEZA


HUYU bibie anatajwa kuwa ndiye mrembo pekee kutoka mjini Tanga aliyefanikiwa angalau kufika tatu bora katika ngazi ya Kitaifa kwenye mashindano ya Miss Tanzania. Mabibi na mabwana ...huyu ni Mona Koja, Miss Tanzania namba 3, wa mwaka 1996 hapo akiwa na mwanae Ryan. Ingawa Rekodi hiyo ya aina yake mpaka sasa bado haijavunjwa na washiriki yeyote kutoka mjini hapa, imani kubwa ipo kuwa Tanga Tunaweza.

Ingawa Mona hakuvikwa taji la Miss Tanzania, lakini alileta upinzani mkubwa katika mashindano hayo mwaka huo na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu ikiwa ni mara ya kwanza mrembo kutoka Tanga kushika nafasi hiyo, tangu mwaka 1994 ambapo shindano hilo lilipanua utafutwaji wa warembo katika ngazi za Mikoa.

Mrembo huyo ambaye amehamishia makazi yake Uingereza alirudi nchini Desemba 24 mwaka jana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya 5Brotherz, alichochangia tunaimani kitasaidia kwenye mchakato mzima wa mishe mishe zetu.

ZAWADI YA MISS TANGA


Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya urembo mkoani Tanga, Mshindi atajinyakulia zawadi ya gari.
Fagilia basi .....

TATU BORA YA MISS VYUO


Hawa ndio walioshika mataji ya miss vyuo, kitongoji kimoja wapo cha miss Tanga 2007
Kati kati anaitwa Victoria Martin ndiye mshindi wa miss vyuo, wa pili kushoto anaitwa Time salum watatu ni Hele Cisary

TANGAZO


Kwa hisani kubwa ya Magazeti ya mwananchi, Tangazo hili limechapishwa humo kwa takriban wiki 6

MCHUANO UKO HIVI


Unadhani nani ataondoka na taji la miss tanga 2007 kati ya hawa?

Sunday, May 20, 2007

MISS COLLAGE KAPATIKANA


Haya tena jamani, hiki ni kitongoji kimoja wapo katika mchakato wa kumpata miss tanga, 'Miss collage' ambapo washiriki kutoka vyuo mbalimbali walichuana.

Katikati niye mshindi anaitwa Victoria Martin, wa pili kuchoto ni Time Salim, watatu ni Helen Cesary. Vicky alishinda kutokana na vigezo muhimu kama unavyomcheki hapo chini lakini pia kujiamini na kujbu swali ipasavyo vilimuongezea point.

toa maoni yako....

Tuesday, May 15, 2007

VISU VYA UHAKIKA




Kila siku zinavyosonga mbele ndivyo mambo yanazidi kuongezeka, hapa tunazungumzia mchakato mzima wa kumpata mrembo mwenye viwango kutoka jijini Tanga.
Habari zilizopo ni kwamba baada ya kitongoji cha miss Chumbageni kwenda vizuri, mazoezi ya Vimwana watakaoshiriki shindano la kumsaka Kisura wa Vyuo jijini Tanga (Miss Collage City Centre)yanaendelea katika ukumbi wa Splended wa Jijini hapa na kua kivutio kutokana na mvuto wa warembo shiriki.

Mratibu wa mashindano hayo ya Miss Collage, Maximilian Luhanga anasema kuwa mvuto wa michuano hiyo umetokana na ubunifu wa mwalimu wao pamoja na mipango thabiti ya waandaaji wakishirikiana na kamati nzima ya Miss Tanga.

Miss Collage atapatikana May 18 katika ukumbi wa Habours Club Jijini, Tayari kwa kuingia katika orodha ya watakao wania taji kubwa la mkoa, Miss Tanga 2007 lililopangwa kufanyika June 8 mwaka huu.


MISS TANGA 2007


Mchuano wa Miss Tanga 2007 Umedhaminiwa na Vodacom, Redds, CRDB, Tanga Fresh, Tanga Uwasa, Screen Masterz, Hotel Kola Prieto, Dollywood, GMC wasanii Promotors, Kampuni ya Mwananchi Communication na Radio Clouds Fm.

WANAUME HALISI



Tumepania jamani

Tuesday, May 8, 2007

MTANGAZAJI AWA MISS CHUMBAGENI 2007


Haya Jamani, katikati ndiye Miss wa kwanza kupatikana kutoka Tanga, Bibie ni mtangazaji wa Televisheni, kwa jina anaitwa Mary Damian Mwita (21). Mary alishinda taji la Kitongoji cha Miss Chumbageni 2007 juzi (May 4) baada ya kuwabwaga vimwana wengine 9.

Mary alifanikiwa kuchomoza katika mchuano huo kufuatia kushinda vigezo mbalimbali lakini kilichompa ushindi ni namna alivyomudu kujibu swali lililoulizwa na Majaji kwa ufundi mkubwa. Aliulizwa endapo angepata bahati ya kukutana na kiongozi yeyote duniani angependa kukutana na nani na angezungumza naye kuhusu nini?. Mrembo huyo alijibu kuwa angependa kuonana na Rais George Bush wa Marekani ambaye angeweza kuzungumza naye kuhusu vita ya Iraki, alisema "Ningetumia fursa hiyo kumshauri asitishe mapigano nchini humo kwa kuwa watu wasio na hatia kama vile watoto, wanawake na wazee wanakufa bila hatia,"

Mary ni mtangazaji wa vipindi mbalimbali katika Televisheni ya Jiji la Tanga (TaTV) fani ambayo aliichukulia katika chuo cha uandishi wa Habari cha Royal Collage mwaka 2005 hadi 2007.

Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Rukia Jumbe (19) mtaalamu wa Hotel Management ambaye alijibu kuwa angependa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kimoon na kumshauri kuweka msukumo zaidi katika mataifa ya Afrika ili nayo yapige hatua za kimaendeleo.


Salma Butenge(Kwenye kapicha hako) alishika nafasi ya tatu katika shindano hilo ambaye alijibu swali hilo kwa kusema angependa kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili azungumze naye juu ya usimamizi duni wa misaada inayotolewa kwa watu mbalimbali wakiwamo yatima na waathirika wa ukimwi.

Aliyenyakua ushindi wa kimwana mwenye kipaji (Miss Tallent Chumbageni 2007 ni Hilda Thomas ambaye aliweza kuvuta hisia za mashabiki waliohudhulia shindano hilo kwa kunengua kisawa sawa wimbo wa Segere wenye mahadhi ya kabila la Kizaramo huku nafasi ya nne ikienda kwa Lina George.

Shindano la Miss Chumbageni 2007 lilitayarishwa na Kampuni ya J.E na kushirikisha jumla ya warembo 16. Mratibu wa michuano hiyo, Juliana Kulangwa aliipongeza kamati ya Miss Tanga 2007 kwa kuonyesha ushirikiano uliowezesha kupata ufanisi. Alisema “Nachukua fursa hii kuwapongeza pia majaji wa shindano hili kwa kutofanya upendeleo, hakukuwa na malalamiko wala manung’uniko kutoka kwa mashabiki” Majaji walifanya kazi hiyo ni Yussuph El Siagi, Minja kutoka kampuni ya Vodacom, Tabu Ruhina na Mwanaidi Mohamed.
- Habari na Buruhani Yakub

MISS TANGA 2007

Tuesday, April 24, 2007

TAARIFA YA MKURUGENZI



MASHINDANO ya urembo kumsaka kisura wa Tanga (Miss Tanga 2007) yatakujia kupitia kampuni ya Five Brothers Entertainment ya hapa jijini Tanga. Kampuni hii inachukua jukumu hili zito ikiwa ni mara ya tatu katika historia yake. Lengo letu ni kuonyesha utofauti uliopo kutoka kwetu na wengine na safari hii tunataka kuhakikisha kuwa Tanga inatoa wawakilishi walioandaliwa vema, wanaoweza kutoa changamoto katika mashindano ya dunia. Ni kweli tumedhamiria kushinda taji la taifa na mrembo wetu kufanya maajabu ambayo hayajawahi kufanywa katika Miss World 2007.

Malengo haya ni mazito na hayawezi kukamilika bila ushirikiano wako wewe. Kwanza kabisa binti yeyote mwenye kipaji na mwenye nia ya kufanya maisha katika fani ya urembo. Pili, familia ya binti huyo kwa kutoa sapoti kwa binti yako kushiriki katika kufanikisha azma ya kipaji chake. Tatu, kwako wewe mwanajamii wa Tanga na vitongoji vyake, kushirikiana nasi kuanzia zoezi la kuwapata wawakilishi toka unapoishi na pia kuingia katika kumbi za kuwaandaa na kupata burudani mbalimbali ambazo tutakuandalia kwa ubora wa kutosha.

Kampuni ya Five Brothers Entertainment inahusika na utayarishaji wa matamasha mbalimbali. Tuna uzoefu katika shughuli hizi hapa nchini na hii ni fursa adimu na muhimu kwako mkazi wa Tanga kushiririkiana nasi, kufahamiana nasi na pia kupata kazi za matunda ya kampuni yetu. Huu ni mwanzo mwema wa kujenga ushirikiano wetu kwako na kwako kwetu. Tunaamini kuwa ushirikiano huu utazidi kuanzia hapa ambapo utapata fursa ya kutumia huduma zetu na sisi kuendelea kukuthamini kama mtumiaji huduma mwenye taadhima zote.

Shangamoto ni kwa Wadhamini wa shughuli hizi, wakati bendera ya mrembo wetu ikipepea, nao watapepea pia, tunapenda kuwashukuru wadhamini wetu wote, Vodacom Tanzania, ambao ndio Main sponsor, Redds, CRDB Bank, Tanga Fresh, Tanga-Uwasa, GMC Wasanii Promotors, Mwananchi Communications, Clouds FM na Hotel Kola Prieto kwa mchango wao.

Kupitia Gazeti Tando hili, tutatoa fursa kwako kutoa maoni ya mambo mbalimbali. Inaweza kuwa, kutuomba tuwashauri mabinti unaowafahamu ili washiriki katika shindano hili, inaweza kuwa maoni kwa ajili ya mazoezi yetu na pia tutakupa kila hatua ya shindano hili kupitia blog hii. Kama utakuwa na maswali kwa washiriki au sisi waandaaji utatakiwa kutoa maswali yako pia hapa ukifuatia njia nyingine kama simu, e-mail na barua.

Ninakukaribisha sana, shiriki nasi katika kuipa Tanga ramani yake ya heshima hapa Tanzania na duniani. Ahsante!

Friday, April 20, 2007

TANGA KUNANI...!!!!!?


TANGA ni mkoa wenye historia nyingi za mambo ya kale yakiwemo ya ajabu na kuvutia ambayo kama yatatangazwa, yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wake. Kwa mujibu wa mtaalamu wa mambo ya kale, Kassim Litinya, karibu kila wilaya kati ya nane zilizoko katika mkoa wetu kuna sehemu hizo za kitalii ambazo baadhi yake bado hazijagundulika na kuendelezwa.

Baadhi ya maeneo hayo ni Tanga mjini yalipo Mapango ya Amboni yanayoaminika kuwepo karne nyingi zilizopita ambayo wakati wa utawala wa Kijerumani yalitumika kama maficho ya mpiganaji Osale Otang na mshirika wake Paul Hamisi aliyekuwa mkazi wa Mkoa wa Tanga. Licha ya mapango hayo ya aina yake kutumika kama maficho ya watu hao, baadhi ya wakazi wa Tanga na hata kutoka nje walikuwa wakiyatumia kwa matambiko na shughuli nyingine za kuabudu mizimu hadi leo hii.


Vile vile katika Mapango hayo ya Amboni kuna michoro inayoonekana ambayo ni matokeo ya miamba kuliwa na maji na kuacha sura na maumbile tofauti tofauti, kama picha za sanamu ya Bikira Maria, picha ya simba, unyayo wa mtu, mkono, ramani ya Afrika na vitu vingine vingi vya ajabu ambavyo vingine husababishwa na muundo wa miamba.

Maeneo mengine ya kihistoria yaliyopo katika Mkoa wa Tanga ni Tongoni Ruins na mji wote wa Pangani, hali kadhalika Wilaya ya Kilindi ambako yamegundulika mapango ya ajabu kwenye mwamba mgumu, sehemu nyingine ni Korogwe ambako kuna msitu wa hifadhi unayoonyesha Jiji zima la Tanga. Pia kuna Magamba Rain Forest-Korogwe yaliko mahandaki ya wajerumani.



Zipo hifadhi za Taifa za Saadani na Mkomazi zilizopo Wilaya za Handeni na Korogwe, Kijiji cha Magila katika Wilaya ya Muheza ambako historia inaeleza kulikuwepo na ma'Chief waliopata heshima kubwa katika jamii nyakati na chemchem ya maji moto.

Kipo Kisiwa cha Totten ambacho kinaaminika kuwepo tangu karne ya 13 iliyopita na awali kilikuwa rasi iliyojulikana kwa jina la Kihongwe katika Mji wa Amboni na watu waliokuwa wakiishi hapo ni wenyeji wa kabila la Wabondei. Asili ya Mji wa Tanga ni Kisiwa hicho cha Totten ambacho kina makaburi ya watu wa kale yakiwemo ya Wajerumani waliokufa tangu miaka ya 1894, visima virefu vya maji na misikiti na pia Katika kisiwa hiki kuna gereza ambalo lilikuwa mahsusi kwa ajili ya watu watukutu na wenye maradhi ya kuambukiza ambao walitengwa huko ili wasije kuambukiza wengine, hapo pia kuna nyumba za askari na ghati la meli za Waarabu na mambo mengine mengi ya ajabu.


Ni mji wa Tanga pekee uliojaaliwa na mkondo wa salfa wa Amboni (Amboni Sulphur Belt) ambao watu mbalimbali hufika na kuoga maji yake kwa ajili ya tiba ya magonjwa ya ngozi kama upele, mapunye na mba, utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa mkondo huo unatokana na mlipuko wa volkano ambayo ndani yake kuna mchanganyiko wa salfa ya asili inayotibu maradhi hayo ya ngozi. Lakini pia baadhi ya watu pia hufika kwa ajili ya matambiko wakiamini kupona.


Ni kama vile haitoshi, yapo pia maporomoko ya maji 'Soni Water Falls' na mambo mengine mazuri ambayo huwezi kuyapata popote isipokuwa Tanga. Kifupi Tanga Rahaaaa! .

Kwa kutambua yote hayo Five Brothers ina mpango kamambe wa utoaji wa elimu ya Hifadhi kwa vijana kupitia mashindano ya Miss Tanga 2007 na mikakati mingine njia ambayo tunaimani kwamba licha ya kuwawezesha vijana kushiriki katika kuzitangaza rasilimali za mkoa, mkakati huo utasaidia kuongeza ajira, na kuamsha ari ya kupenda asili yetu.