Tuesday, April 24, 2007

TAARIFA YA MKURUGENZI



MASHINDANO ya urembo kumsaka kisura wa Tanga (Miss Tanga 2007) yatakujia kupitia kampuni ya Five Brothers Entertainment ya hapa jijini Tanga. Kampuni hii inachukua jukumu hili zito ikiwa ni mara ya tatu katika historia yake. Lengo letu ni kuonyesha utofauti uliopo kutoka kwetu na wengine na safari hii tunataka kuhakikisha kuwa Tanga inatoa wawakilishi walioandaliwa vema, wanaoweza kutoa changamoto katika mashindano ya dunia. Ni kweli tumedhamiria kushinda taji la taifa na mrembo wetu kufanya maajabu ambayo hayajawahi kufanywa katika Miss World 2007.

Malengo haya ni mazito na hayawezi kukamilika bila ushirikiano wako wewe. Kwanza kabisa binti yeyote mwenye kipaji na mwenye nia ya kufanya maisha katika fani ya urembo. Pili, familia ya binti huyo kwa kutoa sapoti kwa binti yako kushiriki katika kufanikisha azma ya kipaji chake. Tatu, kwako wewe mwanajamii wa Tanga na vitongoji vyake, kushirikiana nasi kuanzia zoezi la kuwapata wawakilishi toka unapoishi na pia kuingia katika kumbi za kuwaandaa na kupata burudani mbalimbali ambazo tutakuandalia kwa ubora wa kutosha.

Kampuni ya Five Brothers Entertainment inahusika na utayarishaji wa matamasha mbalimbali. Tuna uzoefu katika shughuli hizi hapa nchini na hii ni fursa adimu na muhimu kwako mkazi wa Tanga kushiririkiana nasi, kufahamiana nasi na pia kupata kazi za matunda ya kampuni yetu. Huu ni mwanzo mwema wa kujenga ushirikiano wetu kwako na kwako kwetu. Tunaamini kuwa ushirikiano huu utazidi kuanzia hapa ambapo utapata fursa ya kutumia huduma zetu na sisi kuendelea kukuthamini kama mtumiaji huduma mwenye taadhima zote.

Shangamoto ni kwa Wadhamini wa shughuli hizi, wakati bendera ya mrembo wetu ikipepea, nao watapepea pia, tunapenda kuwashukuru wadhamini wetu wote, Vodacom Tanzania, ambao ndio Main sponsor, Redds, CRDB Bank, Tanga Fresh, Tanga-Uwasa, GMC Wasanii Promotors, Mwananchi Communications, Clouds FM na Hotel Kola Prieto kwa mchango wao.

Kupitia Gazeti Tando hili, tutatoa fursa kwako kutoa maoni ya mambo mbalimbali. Inaweza kuwa, kutuomba tuwashauri mabinti unaowafahamu ili washiriki katika shindano hili, inaweza kuwa maoni kwa ajili ya mazoezi yetu na pia tutakupa kila hatua ya shindano hili kupitia blog hii. Kama utakuwa na maswali kwa washiriki au sisi waandaaji utatakiwa kutoa maswali yako pia hapa ukifuatia njia nyingine kama simu, e-mail na barua.

Ninakukaribisha sana, shiriki nasi katika kuipa Tanga ramani yake ya heshima hapa Tanzania na duniani. Ahsante!

Friday, April 20, 2007

TANGA KUNANI...!!!!!?


TANGA ni mkoa wenye historia nyingi za mambo ya kale yakiwemo ya ajabu na kuvutia ambayo kama yatatangazwa, yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wake. Kwa mujibu wa mtaalamu wa mambo ya kale, Kassim Litinya, karibu kila wilaya kati ya nane zilizoko katika mkoa wetu kuna sehemu hizo za kitalii ambazo baadhi yake bado hazijagundulika na kuendelezwa.

Baadhi ya maeneo hayo ni Tanga mjini yalipo Mapango ya Amboni yanayoaminika kuwepo karne nyingi zilizopita ambayo wakati wa utawala wa Kijerumani yalitumika kama maficho ya mpiganaji Osale Otang na mshirika wake Paul Hamisi aliyekuwa mkazi wa Mkoa wa Tanga. Licha ya mapango hayo ya aina yake kutumika kama maficho ya watu hao, baadhi ya wakazi wa Tanga na hata kutoka nje walikuwa wakiyatumia kwa matambiko na shughuli nyingine za kuabudu mizimu hadi leo hii.


Vile vile katika Mapango hayo ya Amboni kuna michoro inayoonekana ambayo ni matokeo ya miamba kuliwa na maji na kuacha sura na maumbile tofauti tofauti, kama picha za sanamu ya Bikira Maria, picha ya simba, unyayo wa mtu, mkono, ramani ya Afrika na vitu vingine vingi vya ajabu ambavyo vingine husababishwa na muundo wa miamba.

Maeneo mengine ya kihistoria yaliyopo katika Mkoa wa Tanga ni Tongoni Ruins na mji wote wa Pangani, hali kadhalika Wilaya ya Kilindi ambako yamegundulika mapango ya ajabu kwenye mwamba mgumu, sehemu nyingine ni Korogwe ambako kuna msitu wa hifadhi unayoonyesha Jiji zima la Tanga. Pia kuna Magamba Rain Forest-Korogwe yaliko mahandaki ya wajerumani.



Zipo hifadhi za Taifa za Saadani na Mkomazi zilizopo Wilaya za Handeni na Korogwe, Kijiji cha Magila katika Wilaya ya Muheza ambako historia inaeleza kulikuwepo na ma'Chief waliopata heshima kubwa katika jamii nyakati na chemchem ya maji moto.

Kipo Kisiwa cha Totten ambacho kinaaminika kuwepo tangu karne ya 13 iliyopita na awali kilikuwa rasi iliyojulikana kwa jina la Kihongwe katika Mji wa Amboni na watu waliokuwa wakiishi hapo ni wenyeji wa kabila la Wabondei. Asili ya Mji wa Tanga ni Kisiwa hicho cha Totten ambacho kina makaburi ya watu wa kale yakiwemo ya Wajerumani waliokufa tangu miaka ya 1894, visima virefu vya maji na misikiti na pia Katika kisiwa hiki kuna gereza ambalo lilikuwa mahsusi kwa ajili ya watu watukutu na wenye maradhi ya kuambukiza ambao walitengwa huko ili wasije kuambukiza wengine, hapo pia kuna nyumba za askari na ghati la meli za Waarabu na mambo mengine mengi ya ajabu.


Ni mji wa Tanga pekee uliojaaliwa na mkondo wa salfa wa Amboni (Amboni Sulphur Belt) ambao watu mbalimbali hufika na kuoga maji yake kwa ajili ya tiba ya magonjwa ya ngozi kama upele, mapunye na mba, utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa mkondo huo unatokana na mlipuko wa volkano ambayo ndani yake kuna mchanganyiko wa salfa ya asili inayotibu maradhi hayo ya ngozi. Lakini pia baadhi ya watu pia hufika kwa ajili ya matambiko wakiamini kupona.


Ni kama vile haitoshi, yapo pia maporomoko ya maji 'Soni Water Falls' na mambo mengine mazuri ambayo huwezi kuyapata popote isipokuwa Tanga. Kifupi Tanga Rahaaaa! .

Kwa kutambua yote hayo Five Brothers ina mpango kamambe wa utoaji wa elimu ya Hifadhi kwa vijana kupitia mashindano ya Miss Tanga 2007 na mikakati mingine njia ambayo tunaimani kwamba licha ya kuwawezesha vijana kushiriki katika kuzitangaza rasilimali za mkoa, mkakati huo utasaidia kuongeza ajira, na kuamsha ari ya kupenda asili yetu.