
TANGA ni mkoa wenye historia nyingi za mambo ya kale yakiwemo ya ajabu na kuvutia ambayo kama yatatangazwa, yanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wake. Kwa mujibu wa mtaalamu wa mambo ya kale, Kassim Litinya, karibu kila wilaya kati ya nane zilizoko katika mkoa wetu kuna sehemu hizo za kitalii ambazo baadhi yake bado hazijagundulika na kuendelezwa.
Baadhi ya maeneo hayo ni Tanga mjini yalipo Mapango ya Amboni yanayoaminika kuwepo karne nyingi zilizopita ambayo wakati wa utawala wa Kijerumani yalitumika kama maficho ya mpiganaji Osale Otang na mshirika wake Paul Hamisi aliyekuwa mkazi wa Mkoa wa Tanga. Licha ya mapango hayo ya aina yake kutumika kama maficho ya watu hao, baadhi ya wakazi wa Tanga na hata kutoka nje walikuwa wakiyatumia kwa matambiko na shughuli nyingine za kuabudu mizimu hadi leo hii.

Vile vile katika Mapango hayo ya Amboni kuna michoro inayoonekana ambayo ni matokeo ya miamba kuliwa na maji na kuacha sura na maumbile tofauti tofauti, kama picha za sanamu ya Bikira Maria, picha ya simba, unyayo wa mtu, mkono, ramani ya Afrika na vitu vingine vingi vya ajabu ambavyo vingine husababishwa na muundo wa miamba.
Maeneo mengine ya kihistoria yaliyopo katika Mkoa wa Tanga ni Tongoni Ruins na mji wote wa Pangani, hali kadhalika Wilaya ya Kilindi ambako yamegundulika mapango ya ajabu kwenye mwamba mgumu, sehemu nyingine ni Korogwe ambako kuna msitu wa hifadhi unayoonyesha Jiji zima la Tanga. Pia kuna Magamba Rain Forest-Korogwe yaliko mahandaki ya wajerumani.

Zipo hifadhi za Taifa za Saadani na Mkomazi zilizopo Wilaya za Handeni na Korogwe, Kijiji cha Magila katika Wilaya ya Muheza ambako historia inaeleza kulikuwepo na ma'Chief waliopata heshima kubwa katika jamii nyakati na chemchem ya maji moto.
Kipo Kisiwa cha Totten ambacho kinaaminika kuwepo tangu karne ya 13 iliyopita na awali kilikuwa rasi iliyojulikana kwa jina la Kihongwe katika Mji wa Amboni na watu waliokuwa wakiishi hapo ni wenyeji wa kabila la Wabondei. Asili ya Mji wa Tanga ni Kisiwa hicho cha Totten ambacho kina makaburi ya watu wa kale yakiwemo ya Wajerumani waliokufa tangu miaka ya 1894, visima virefu vya maji na misikiti na pia Katika kisiwa hiki kuna gereza ambalo lilikuwa mahsusi kwa ajili ya watu watukutu na wenye maradhi ya kuambukiza ambao walitengwa huko ili wasije kuambukiza wengine, hapo pia kuna nyumba za askari na ghati la meli za Waarabu na mambo mengine mengi ya ajabu.

Ni mji wa Tanga pekee uliojaaliwa na mkondo wa salfa wa Amboni (Amboni Sulphur Belt) ambao watu mbalimbali hufika na kuoga maji yake kwa ajili ya tiba ya magonjwa ya ngozi kama upele, mapunye na mba, utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa mkondo huo unatokana na mlipuko wa volkano ambayo ndani yake kuna mchanganyiko wa salfa ya asili inayotibu maradhi hayo ya ngozi. Lakini pia baadhi ya watu pia hufika kwa ajili ya matambiko wakiamini kupona.

Ni kama vile haitoshi, yapo pia maporomoko ya maji 'Soni Water Falls' na mambo mengine mazuri ambayo huwezi kuyapata popote isipokuwa Tanga. Kifupi Tanga Rahaaaa! .
Kwa kutambua yote hayo Five Brothers ina mpango kamambe wa utoaji wa elimu ya Hifadhi kwa vijana kupitia mashindano ya Miss Tanga 2007 na mikakati mingine njia ambayo tunaimani kwamba licha ya kuwawezesha vijana kushiriki katika kuzitangaza rasilimali za mkoa, mkakati huo utasaidia kuongeza ajira, na kuamsha ari ya kupenda asili yetu.

No comments:
Post a Comment