
Haya Jamani, katikati ndiye Miss wa kwanza kupatikana kutoka Tanga, Bibie ni mtangazaji wa Televisheni, kwa jina anaitwa Mary Damian Mwita (21). Mary alishinda taji la Kitongoji cha Miss Chumbageni 2007 juzi (May 4) baada ya kuwabwaga vimwana wengine 9.
Mary alifanikiwa kuchomoza katika mchuano huo kufuatia kushinda vigezo mbalimbali lakini kilichompa ushindi ni namna alivyomudu kujibu swali lililoulizwa na Majaji kwa ufundi mkubwa. Aliulizwa endapo angepata bahati ya kukutana na kiongozi yeyote duniani angependa kukutana na nani na angezungumza naye kuhusu nini?. Mrembo huyo alijibu kuwa angependa kuonana na Rais George Bush wa Marekani ambaye angeweza kuzungumza naye kuhusu vita ya Iraki, alisema "Ningetumia fursa hiyo kumshauri asitishe mapigano nchini humo kwa kuwa watu wasio na hatia kama vile watoto, wanawake na wazee wanakufa bila hatia,"
Mary ni mtangazaji wa vipindi mbalimbali katika Televisheni ya Jiji la Tanga (TaTV) fani ambayo aliichukulia katika chuo cha uandishi wa Habari cha Royal Collage mwaka 2005 hadi 2007.

Mshindi wa pili katika shindano hilo ni Rukia Jumbe (19) mtaalamu wa Hotel Management ambaye alijibu kuwa angependa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kimoon na kumshauri kuweka msukumo zaidi katika mataifa ya Afrika ili nayo yapige hatua za kimaendeleo.

Salma Butenge(Kwenye kapicha hako) alishika nafasi ya tatu katika shindano hilo ambaye alijibu swali hilo kwa kusema angependa kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili azungumze naye juu ya usimamizi duni wa misaada inayotolewa kwa watu mbalimbali wakiwamo yatima na waathirika wa ukimwi.
Aliyenyakua ushindi wa kimwana mwenye kipaji (Miss Tallent Chumbageni 2007 ni Hilda Thomas ambaye aliweza kuvuta hisia za mashabiki waliohudhulia shindano hilo kwa kunengua kisawa sawa wimbo wa Segere wenye mahadhi ya kabila la Kizaramo huku nafasi ya nne ikienda kwa Lina George.
Shindano la Miss Chumbageni 2007 lilitayarishwa na Kampuni ya J.E na kushirikisha jumla ya warembo 16. Mratibu wa michuano hiyo, Juliana Kulangwa aliipongeza kamati ya Miss Tanga 2007 kwa kuonyesha ushirikiano uliowezesha kupata ufanisi. Alisema “Nachukua fursa hii kuwapongeza pia majaji wa shindano hili kwa kutofanya upendeleo, hakukuwa na malalamiko wala manung’uniko kutoka kwa mashabiki” Majaji walifanya kazi hiyo ni Yussuph El Siagi, Minja kutoka kampuni ya Vodacom, Tabu Ruhina na Mwanaidi Mohamed.
- Habari na Buruhani Yakub
MISS TANGA 2007